Baada ya Mshambuliaji kutoka DR Congo Jean Baleke kuibeba Simba SC kwa kuifungia mabao matatu ‘Hat Trick’ dhidi ya Mtibwa Sugar, Benchi la Ufundi la timu hiyo kupitia kwa Kocha Msaidizi, Juma Ramadhan Mgunda umetamba kuwa mchezaji ni miongoni mwa wachezaji hatari na wanataka kuona anacheza kwenye kiwango hicho dhidi ya Mabingwa wa Soka nchini Guinea Horoya AC.

Baleke juzi Jumamosi (Machi 11) alifunga ‘Hat Trick’ yake ya kwanza akiwa na Simba SC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo walioshinda mabao 3-0.

Baada ya mchezo huo Simba SC walifikisha alama 57 na kuendelea kusalia nafasi ya pili ya msimamo, wakitanguliwa na Watani zao wa Jadi Young Africans waliofikisha alama 65, baada ya kushinda mchezo wa jana Jumapili (Machi 12) dhidi ya Geita Gold FC.

Simba SC itakutana na Horoya AC katika mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Jumamosi (Machi 18) ambao utapigwa kwenye Uwanja wa Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.

Kocha Mgunda amesema: “Tumefurahishwa na namna ambavyo kikosi chetu kilicheza mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar na kufanikiwa kupata pointi tatu muhimu lakini pia tumefurahishwa na kiwango alichoonyesha Baleke.”

“Ni miongoni mwa washambuliaji bora kwenye kikosi chetu, lakini unajua hivi karibuni alishindwa kufunga katika mechi kadhaa na kwa kiasi fulani ni kama alipoteza kujiamini, tulikaa naye chini na tunaamini ataendelea kuonyesha kiwango bora kuelekea mechi zijazo ikiwemo mchezo dhidi ya Horoya Jumamosi.”

Wakuu wa Wilaya watakiwa kuzingatia utawala bora
Young Africans kuivaa US Monastir kivingine