Mshambuliaji wa klabu bingwa nchini Ufaransa Paris Saint-Germain (PSG) Neymar da Silva Santos Júnior amekabidhiwa jumla jukumu la kuwa nahodha wa timu ya taifa ya Brazil, chini ya utawala wa kocha Adenor Leonardo Bacchi (Tite).
Kocha Tite amemtangaza rasmi mshambuliaji huyo katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Marekani, utakaochezwa baadae hii leo mjini New Jersey-Marekani.
Kocha Tite amefuta mfumo wa kutokua na nahodha maalum katika kikosi chake, na anaamini mshambuliaji huyo wa PSG anatosha kuwa kiongozi wa wachezaji wengine katika kikosi cha Brazil.
“Nimefuta mpango wa kuwatumia wachezjai wangu kadhaa kama manahodha wa kikosi, nimefanya maamuzi ya kumteua Neymar kuwa nahodha wa kudumu wa kikosi, katika kipindi chote nitakachokua kocha mkuu wa Brazil.” Alisema Tite.
“Imenichukua muda mrefu kutafakari suala hili, na nimeona Neymar anafaa kutokana na baadhi ya tabia nilizoziona kwake, ninatarajia mazuri na ushirikiano mkubwa kutoka kwake dhidi ya wachezaji wengine ili kufikia lengo la kufanya vizuri katika michezo inayotukabili.”
Kwa upande wa Neymar ambaye alishiriki katika mkutano na waandishi wa habari sambamba na kocha Tite, amesema amelipokea jukumu hilo kwa mikoni miwili, na atalifanyia kazi kwa vitendo akiwa nje na ndani ya uwanja.
“Nimelikubali jukumu hili, japo ni zito kutokana na umri wangu, nitajitahidi kufanya linalowezekana kuwaongoza wenzangu na kufikia lengo la kufanya vizuri kila tunapocheza dhidi ya wapinzani.”
“Najua ilikua ni nafasi ya kila mmoja wetu kukabidhiwa jukumu la kuwa nahodha wa kikosi, lakini kocha ameniteua mimi, sina budi kulikubalia na kuangalia namna ya kusaidiana naye katika majukumu ya kufanikisha lengo linalokusudiwa hapa.”
Kuhusu kutofikia lengo katika fainali za kombe la dunia 2018 Neymar amesema: “Niwaombe radhi mashabiki wetu waliokwazika na kilichotokea nchini Urusi, ni sehemu ya matokeo na hatukupenda kutolewa katika hatua ya robo fainali, tunaamini wakati mwingine tutafanya vizuri ziadi.”
Baada ya kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Marekani baadae hii leo, kikosi cha Brazil kitapambana na El Salvador katika mchezo mwingine wa kirafiki mwanzoni mwa juma lijalo.