Kocha wa Mabingwa wa Soka nchini Uganda Vipers Roberto Luiz Bianch Pelliser ameibeza Simba SC, kwa kusema hajaona mchezaji mwenye kipaji ambacho kitakua na madhara kwenye mchezo wa Jumamosi (Februari 25).
Vipers SC itaikaribisha Simba katika Uwanja wa St Marry’s nchini Uganda, kwenye mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ikiwa na alama moja mkononi, huku Mnyama akiambulia patupu hadi sasa.
Kocha Pelliser amesema ameifuatilia Simba SC katika michezo yote miwili ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Horoya AC na ule wa Raja Casablanca, na kubaini udhaifu ambao atautumia kupata alama tatu nyumbani.
“Nimewaona Simba kwenye michezo miwili lakini sijaona mchezaji mwenye kipaji kikubwa cha kutuogopesha Ukilinganisha na Wachezaji wetu, sisi tunaendelea na maandalizi tuna uhakika tutashinda”
“Tutachukua alama 6 kwa Simba SC nina uhakika huo, hata kwa Horoya AC tunaamini tunaweza kupata alama moja nyingine kwao ama kupata zote tatu, halafu baada ya hapo tutajua hatma yetu katika Kundi hili.” amesema Kocha Pelliser
Tayari Simba SC imeanza safari ya kuelekea nchini Uganda leo Alhamis (Februari 23), huku lengo kuu ni kupambana na kupata alama ugenini, kisha kuzipigania nyingine kwenye mchezo ujao utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa mwishoni mwa juma lijalo dhidi ya Vipers SC.
Kabla ya kuanza safari Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC Clatous Chama alizungumza na waandishi wa habari Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julias Nyerere na kueleza namna walivyojipanga, kuelekea mchezo ujao dhidi ya Vipers SC.
Amesema wamejiandaa vizuri, lakini kesho watakamilisha sehemu ya maandalizi ya mchezo huo wakiwa Uganda, hivyo amewataka Mashabiki na Wanachama kuendelea kuiombea timu yao na kuiamini wakati wote.