Serikali imepanga kuboresha uwezo wa Mtandao wa Mawasiliano Serikalini (Government Network) na kuufikisha katika Wilaya zote nchini, ili kurahisisha utekelezaji wa jitihada zake na kuwafikishia huduma wananchi wote.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba hii leo Februari 23, 2023 Jijini Dodoma, wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo.

Amesema mpango mwingine ni kupitia na kutathmini hali ya usalama wa Mifumo na miundombinu ya Serikali Mtandao na kuzishauri Taasisi za Umma katika maeneo ya kuboresha, pamoja na kufuatilia utekelezaji wake, ili kuhakikisha mifumo na miundombinu ya TEHAMA inafanya kazi wakati wote kwa ufanisi na usalama.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba.

“Mamlaka kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Umma, imefanikiwa kutengeneza mifumo mbalimbali ya kisekta inayotumika katika taasisi, ikiwemo mfumo wa ukusanyaji wa Malipo ya Serikali Kielektroniki – GePG uliotengenezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango, mfumo huu unaimarisha uwazi na udhibiti katika ukusanyaji mapato ya Serikali,”amesema.

Akizungumzia mipango ya Mamlaka kwa miaka 10 ijayo, amesema katika kuhakikisha wanaijenga Serikali ya Kidijiti, eGA itaandaa na kutekeleza mikakati madhubuti ili kuimarisha zaidi utekelezaji wa jitihada za Serikali.

“Mamlaka itaandaa uwezo wa kutumia teknolojia mpya zinazoibuka, hasa zile za akili bandia, sarafu za kidijiti na teknolojia za kifedha, ili kuwezesha maboresho ya kiutendaji katika Taasisi za Umma na utoaji wa huduma kwa umma,”amesema.

Kocha Vipres SC aipotezea Simba SC
Wanamshauriwa vibaya Rais: Kitwanga