Ni kama kocha mkuu wa Young Africans ameshaanza kazi pasina kuonekana kwenye Uwanja mazoezi ya kikosi cha timu hiyo, ambayo yameanza jijini Dar es salaam, kwa ajili ya kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2020/21.
Taarifa zinaeleza kuwa huenda kocha mpya wa klabu hiyo akatangzwa na uongozi kupitia vyombo vya habari mwishoni mwa juma hili, huku mzaliwa na Burundi Cedric KAze akitajwa kuwa kwenye mazungumzo ya mwisho kabla ya kukabidhiwa jukumu hilo.
Young Africans ambayo kwa muda mrefu imekuwa sokoni kutafuta kocha mkuu wa kurithi mikoba ya Mbelgiji Luc Eymael aliyetimuliwa baada ya kumalizika msimu wa 2019/20, imeanza mazoezi ikiwa chini ya Kocha wa viungo, rai wa Afrika Kusini, Riedoh Berdien.
Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Wakili Simon Patrick, amewataka Wanayanga kutulia huku akiwaeleza kila kitu kinakwenda vizuri ikiwa ni pamoja na kocha huyo kuanza kazi kwa kutuma programu zake ambazo zinatumika mazoezini kwa sasa.
“Wiki hii watajua kila kitu, na kuhusu mazoezi, tayari ametuma progamu zake ambazo wachezaji wanaendelea nazo kupitia kwa kocha msaidizi,” amesema Simon.
Ingawa mashabiki wa soka wamekuwa wakishangaa na kuhoji usajili unaofanyika bila kocha ikiwa ni pamoja na mazoezi yanayoendelea, lakini habari za uhakika ni kwamba tayari kocha mkuu wa kuinoa timu hiyo ameshapatikana na kuanza kazi kwa kutuma programu ambazo zinatumiwa mazoezini na msaidizi wake, Berdien.
Lakini kwa upande wa Mkurugenzi Mwekezaji wa kampuni ya, Hersi Said, wanaoidhamini Young Africans na ambao wamekuwa mstari wa mbele katika suala nzima la usajili wa wachezaji pamoja na kutafuta kocha, naye amesema watamtangaza rasmi ndani ya juma hili.
Hersi amesema tayari wamempata kocha wa kukinoa kikosi hicho na kwa sasa anasubiri vipimo vya corona (COVID-19) kutoka ili kuweza kupata kibali cha kusafiri.
Alipotajiwa jina la Mrundi Cedric Kaze, anayetajwa kuwa ndiye atakayekinoa kikosi hicho, Hersi amesema “haupo mbali” huku akieza kwamba kwa sasa kocha wao yupo Amerika Kusini.
“Kilichomchelewesha kutua ni kutokana na kusubiri vipimo vya COVID-19, lakini jumaili haliishi anaweza kuwasili na tutamtangaza rasmi, hivyo Wanayanga wasubiri mambo mazuri yanakuja,” amesema.