Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la mpira wa Miguu la Misri (EFA), Ahmed Shobir amesema kombe la AFCON limepotea katika makao makuu ya Shirikisho hilo.
Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON lilikuwa limehifadhiwa Misri baada ya timu ya Pharaohs kushinda kwa mara tatu mfululizo tangu mwaka 2006 hadi 2010.
Imesemekana kuwa EFA ilitaka kuweka medali na kombe hilo katika makao makuu ya ofisi zake siku ambayo wangesheherekea mwaka wa 100 wa kuanzishwa kwa shirikisho hilo, ndipo walipogundua kombe halipo.
Watendaji wa Shirikisho hilo wamedai ya kuwa kombe hilo lilikuwa limehifadhiwa kwa nahodha wa timu ya taifa, Ahmed Hassan.
Hassan amekanusha hilo na kusema alikaa nalo kwa siku moja tu baada ya kushinda na alikabidhi tangu mwaka 2011.