Wadhamini Wakuu wa Ligi Kuu Tanzania Bara Benki ya NBC leo Alhamis (Juni 09) wamelianika hadharani Kombe la Ubingwa wa Ligi hiyo msimu huu 2021/22, ambao utafikia ukingoni baadae mwezi huu.
NBC inayodhamini Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza msimu huu 2021/22, imefanya tukio hilo katika Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Dar es salaam katika hafla maalum, ambayo ilihudhuriwa na maafisa wa Benki hiyo, Bodi ya Ligi ‘TPLB’, Wawakilishi wa Vilabu pamoja na Waandishi wa Habari.
Akizungumza katika hafla hiyo Afisa Mtendaji Mkuu wa ‘TPLB’ Almas Kassongo amesema Kombe hilo la ubingwa ambalo lina muonekano wa tofauti, litakua rasmi kwa Bingwa wa kila msimu wa Ligi Kuu, kuanzia msimu huu 2021/22.
Amesema Wadhamini Wakuu Benki ya NBC, pia wamekubali kutengeneza Kombe Mbadala (Bandia) ambalo litabaki kwa kila bingwa wa kila msimu, ili kutoa nafasi ya Kombe halisi kurudishwa kwa wahusika kwa ajili ya Msimu mpya wa Ligi Kuu.
“Kila msimu bingwa atakabidhiwa Kombe halisi katika hafla maalum ya kukabidhi, lakini baada ya hapo tutampatia Kombe Mbadala (Bandia) kwa ajili ya kumbukumbu.”
“Huu umekua ni utaratibu wa dunia nzima kufanya hivyo, kwa hiyo Kombe hili halisi litaendelea kubaki kama lililovyo na litakabidhiwa kwa kila Bingwa wa kila msimu kwa kupokezana, ama kwa Bingwa yuleyule kama atajirudia” amesema Almas Kassongo.
Tayari klabu ya Young Africans imeshaonesha dalili zote za kubwa Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Msimu huu 2021/22, baada ya kubakisha alama tatu kufikia lengo hilo. Klabu ya Young Africans itaweka historia ya kuwa klabu ya kwanza Tanzania Bara kukabidhiwa Kombe la Ubingwa lenye muonekano mpya.