Timu ya taifa ya Jamuhuri Ya Kidemokrasia Ya Kongo usiku wa kuamkia hii leo ilianza vyema kampeni za kuusaka ubingwa wa Afrika kwa mwaka 2017, kwa kupata ushindi dhidi ya Morocco.
Bao lililofungwa na mshambuliaji wa FC Astana ya nchini Kazakhstan Junior Kabananga, lilitosha kuipa kicheko timu hiyo ya rais Kabila, katika mchezo huo ambao ulikua unatabiriwa huenda ungewapa furaha wamorocco.
Kabananga alifunga bao hilo pekee kwa ustadi mkubwa katika dakika ya 55, kwa kuupiga mpira uliokua umegonga mwamba baada ya Firmin Mubele kupiga krosi ambayo ilimshinda mlinda mlango wa Morocco, Munir Mohamedi.
Hata hivyo dakika tisa za mwisho za mchezo huo, kikosi cha Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kilicheza pungufu, kufuatia Joyce Lomalisa kuonyeshwa kadi nyekundu iliyoambatana na kadi mbili za njano.
Morocco walikaribia kupata bao la kusawazisha katika dakika za lala salama, lakini umahiri wa mlinda mlango wa Congo Ley Matampi ulisaidia kuondoa hatari iliyoletwa langoni kwake na Youssef El Arabi.
Wakati huo huo mabingwa watetezi Ivory Coast ambao wamepangwa katika kundi C, walishindwa kufurukuta mbele ya Togo kwa kuambulia sare ya bila kufungana.
Michuano hiyo inaendelea tena hii leo kwa michezo ya kundi D ambapo:
Ghana Vs Uganda ( Saa moja jioni)
Mali Vs Misri (Saa nne Usiku)