Wakati Tabora United wakipata sare ya kwanza nyumbani dhidi ya KMC, kocha Goran Kopunovic amejikuta akishangaa kiwango Cha kikosi chake kisha akateta na wachezaji wake.
Kopunovic amesema amelazimika kuwa mkali kwa wachezaji wake kwa kushindwa kutengeneza nafasi za kufunga lakini pia wakiwa na makosa mengi kwenye safu yao ya ulinzi.
“Hatukucheza kama ambavyo tulicheza mechi nne zilizopita, hatukuonyesha kama tuna njaa ya ushindi, hatukutengeneza nafasi bora za kutosha, hiki ni kiwango cha chini zaidi tangu nimefika hapa.” amesema Kopunovic.
“Hii ni sare ya pili kwetu tukitangulia kupata sare ugenini (dhidi ya Singida Big Stars) lakini nilichukia nikajikuta nakuwa mkali kwa wachezaji wangu tunatakiwa kubadilika kwa kuhakikisha tunalinda muendelezo wetu wa kuwa bora.”
Kocha huyo ameongeza kuwa amelazimika kuwaomba radhi mashabiki wa timu yake ambao walikuja kwa wingi kuishuhudia timu hiyo kwa kukosa matokeo bora huku pia kiwango cha timu kikiwa cha chini.
Amesema kwa sasa wanaanzia kuelekeza akili zao kwenye mechi tatu za ugenini wakianza na JKT Tanzania, Kagera Sugar na Geita Gold ambazo anaamini zitakuwa ngumu.
“Mashabiki wanapokuja kutupa nguvu wanaamini kwamba tutawafurahisha kwa kucheza vizuri na kushinda na hayo yote waliyakosa watusamehe tutarudi kuwa bora zaidi.” amesema.
Tunatakiwa kuwa timamu kwenye mechi zetu tatu zinazokuja zote za ugenini ni ratiba ngumu, tunakwenda kukutana na timu zenye ubora mkubwa, kitu tunachotaka kufanya ni kurudi kwenye ubora wetu.”