Korea Kaskazini imeilaumu Marekani kwa kuchochea mivutano ya kijeshi kutokana na kufanya mazoezi ya kijeshi ya pamoja na Korea Kusini na imesema kuwa itachukua hatua za kujihami.
Balozi wa Korea Kaskazini jijini Geneva amewaambia wajumbe kwenye mkutano juu ya kupunguza silaha unaodhaminiwa na Umoja wa Mataifa kwamba Korea Kaskazini itazifikiria upya hatua ilizochukua hadi sasa.
Aidha, mjumbe wa Marekani kwenye mkutano huo, Robert Wood, amekanusha madai hayo kwa kusema kuwa Marekani haichochei mivutano bali inafanya mazoezi ya kawaida tu ya kijeshi.
Wood ameeleza kuwa Marekani inadhamiria kulitekeleza lengo la kuondolewa silaha za nyuklia za Korea Kaskazini kama jinsi kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong Un, alivyokubaliana na Rais Donald Trump kwenye mkutano wao wa kwanza uliofanyika Singapore mwaka uliopita.
Hata hivyo, Mjumbe huyo wa Marekani amesema kuwa nchi yake inasubiri kwa hamu kubwa kurejea kwenye mazungumzo na Korea Kaskazini ili kulitekeleza lengo lililowekwa kwenye mkutano huo.