Kocha Krasimir Balakov ametangaza kujizulu nafasi ya ukuu wa benchi la ufundi la timu ya taifa ya Bulgaria, kufuatia kadhia ya ubaguzi wa rangi iliyojitokeza wakati wa mchezo kuwania kufuzu fainali za Ulaya (Euro 2020) dhidi ya England uliochezwa mwanzoni mwa juma hili.
Balakov mwenye umri wa miaka 53, ametangaza maamuzi hayo kama kujiwajibisha mwenyewe, kufuatia kauli aliyoitoa baada ya mchezo dhidi ya England kwa kusema hakusikia kelele za ubaguzi wa rangi ambazo zilitolewa na mashabiki, pindi wachezaji wa timu pinzani wenye asili ya Afrika walipogusa mpira.
“Kuanzia leo mimi sio kocha wa timu ya taifa, ninabeba jukumu la kujiuzulu nafasi hii, kwa kuonyesha namna ya kuwajibika kwa makosa yaliyojitokeza wakati wa mchezo wetu dhidi ya England.,” alisema Balakov alipozungumza na waandishi wa habari mjini Sofia, Bulgaria.
“Ninamtakia kila la kheri kocha atakaerithi nafasi yangu, ninaamini atafanikisha mazuri kwa ajili ya timu yetu ya taifa, ambayo siku za karibuni imeshindwa kuonyesha kiwango cha kushindana vilivyo uwanjani.”
“Siwezi kuendelea kuwa kocha kwa hali hii inayoendelea, kwanza suala hili la ubaguzi wa rangi, na pili kushindwa kufikia lengo la kuiwezesha timu kucheza soka la ushindani.”
Kwa mujibu wa taarifa kutoka mjini Sofia zinaeleza kuwa, mbali na kujiuzulu kwa kocha huyo, bodi ya uongozi wa shirikisho la soka Bulgaria nayo imetangaza kujiuzulu akiwepo rais Borislav Mikhailov.
Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA lilithibitisha kuwepo kwa matukio ya ubaguzi wa rangi wakati wa mchezo dhidi ya England, jambo ambalo limedhihirisha kocha Balakov hakuwa sahihi kutoa kauli wa kukana kusikia maneno ya kibaguzi, ambayo imedhihirisha alikua akiunga mkono vitendo viovu vilivyoonyeshwa na mashabiki wa Bulgaria.
Mamlaka za usalama nchini Bulgaria tayari zimeshawati nguvuni mashabiki 12 miongoni mwa mashabiki 16, ambao walidhihirika kufanya vitendo vya ubaguzi wa rangi dhidi ya wachezaji wa England wenye asili ya bara la Afrika.
Tayari mashabiki wanne wameshatozwa faini na kufungiwa miaka miwili kuingia kwenye viwanja vya soka duniani, huku wengine wakiendelea kujitetea na kusubiri hukumu zao.