Mbunge wa Ubungo ,Saed Kubenea amesema anatarajia kuandika barua kwa Msajili wa Vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mutungi pamoja na Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano Tanzania Job Ndugai kuwaelezea jinsi anavyozuiliwa na Jeshi la Polisi kufanya mikutano na shughuli za chama katika jimbo lake.
Kubenea aliyasema hayo jana kwenye mkutano na waandishi wa habari ambapo alilalamikia hatua ya kuzuiwa mikutano na wananchi ili kufanya mambo ya maendeleo.
Aliongeza kuwa kama Msajili na Spika wa Bunge hawatamsikiliza kilio hicho basi atakishawishi chama chake kwenda Umoja wa Mataifa kuelezea yanayowakabili ikiwa ni pamoja na kunyimwa kufanya mikutano na wananchi wake.
Katika hatua nyingine mbunge huyo aligawa vifaa kwa ajili ya uchaguzi wa seikali ya mitaa ikiwa ni pamoja na vitabu na mihuri katika kata 46 za jimbo hilo.
Alisema hata kama Jeshi la Polisi wanawafifiisha katika kufanya kazi lakini watahakikisha wanashinda uchaguzi wa serikali za mitaa.