Mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Burundi aliejiunga na Young Africans siku moja baada ya kuigaragaza Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) SAIDI Ntibazonkiza, ana historia ya kipekee katika soka la ukanda wa Afrika mshariki na kati.
Said Ntibazonkiza, ambaye alithibitishwa kujiunga na Young Africans jioni Oktoba 12 mwaka huu, alizaliwa May Mosi mwaka 1987 katika mji wa Bujumbura-Burundi, na maisha yake ya soka yalianzia kwenye klabu ya Vital’O mwaka 2003 hadi 2004.
Mwaka 2006 alijiunga na NEC Nijmegen ya nchini Uholanzi akianzia kwenye timu ya vijana na mwaka huo huo Novemba 18 akapandishwa timu ya wakubwa ambako alidumu mpaka mwaka 2010 na kufanikiwa kucheza michezo 70 na kupachika mabao 10.
Mwaka 2010 alijiunga na klabu ya KS Cracovia ya nchini Poland ambako alidumu mpaka mwaka 2014 na kufanikiwa kucheza michezo 85 na kutupia mabao 17.
Mwaka 2014 alijunga na klabu ya Akhisar Belediyespor ya nchini Uturuki ambako alidumu mpaka mwaka 2015 na kucheza michezo 13 na kupachika bao 1.
Mwaka 2015 alijiunga na Caen Fc ya nchini Ufaransa ambayo kwa wakati ule ilikuwa inashiriki Ligi Kuu nchini Ufaransa (Ligue 1) na sasa ipo Ligue 2, ambapo huko alipelekwa timu B (Caen B) ambako alicheza michezo minne 4 na kufunga bao moja 1.
Mwaka huo huo 2015 alipandishwa Senior team Caen Fc ambako alidumu mpaka mwaka 2016 na kufanikiwa kucheza michezo 14 na kufunga bao moja 1.
Mwaka 2017 alijunga na klabu ya FC Kaisar ya nchini Khazakistan ambako alicheza msimu mmoja tu na kufanikiwa kucheza michezo 10 na kufunga mabao mawili.
Baadae aliachana na klabu hiyo na kuwa mcheza huru ambapo mwaka 2019 timu yake ya zamani Vital’O iliamua kumrudisha ndani ya kikosi cha warundi hao.
Kwa upande wa timu ya taifa lake la Burundi, alianza kuitumikia timu hiyo mwaka 2010, na amekua nahodha wa kikosi cha Intamba murugamba kuanzia mwaka huo, japo badae alikuja kufungiwa kutoitimikia timu hiyo kuanzia 2015 na baadae alirejeswa kikosini.
Kila la kheir Said Ntibazonkiza katika majukumu yako mapya, Dar24 Media tunakukumbusha kuwa, lengo kuu la klabu yako mpya ni kusaka ubingwa wa Tanzania Bara ambao upo mikononi mwa Wekundi wa Msimbazi kwa misimu mitatu mfululizo.