Uwezeshaji wa wanawake wa vijijini kiuchumi, kijamii, kisiasa, na utamaduni, imetajwa ni moja ya nguzo muhimu ya kuelekea uchumi wa kati wa viwanda.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii na Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Julius Mbilinyi alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya kilele cha siku ya wanawake duniani.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “kuelekea uchumi wa viwanda, tuimarishe usawa wa jinsia na uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake wa vijijni” huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa pamoja na jitihada nyingi zinazofanywa na serikali kuhakikisha taifa linafikia katika uchumi wa kati wa viwanda, lakini kuwawezesha wanawake wa vijijini kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni ni hatua nzuri ya kufikia malengo hayo.
“Wanawake ndio chachu ya maendeleo ya uchumi wa taifa lolote lile, hivyo sisi kama wizara tunaihamasisha jamii kuimarisha usawa wa jinsia na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake hao ili tuweze kufikia malengo,” alisema Mbilinyi.
Alisema pia wakiwezeshwa na kujua haki zao na kuweza kuzitetea katika jamii watakuwa na mchango mkubwa katika taifa kwa kuwa watamudu kufanya shughuli za uzalishaji mali ambazo zitawaongezea kipato wao binafsi lakini kukuza uchumi wao na taifa kwa jumla