Rais wa Rwanda, Paul Kagame amesema kundi la waasi la Democratic Forces for Liberation of Rwanda (FDLR), linaloshutumiwa kusababisha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 linaungwa mkono na baadhi ya watu, kwa lengo la kuipindua Serikali yake.
Kagame ameyasema hayo kupitia hotuba take aliyoitoa kupitia video wakati akiwahutubia Maseneta, bila kutaja majina ya nchi au watu anaodai kwamba wanaliunga mkono kundi la FDLR, na kudai kuwa kundi hilo linajificha katika baadhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Hotuba hiyo, ambayo imewekwa kwenye akaunti rasmi ya mtandao wa YouTube wa Rais Paul Kagame imefafanua kuwa, “Kundi la FDLR ambalo limepewa hifadhi kwa miongo kadhaa nadhani limehifadhiwa kwa makusudi.”
Kagame ameongeza kuwa, “Unaposema kwamba waasi wa M23 na watu wengine ambao unawaondoa – ukisema warudi Rwanda kwa hiari au bila hiari, lakini huzungumzii kuhusu kundi la FDLR kwa sababu unalitaka kuendelea kuwepo hiki ndio kiini cha mzozo.”
Aidha, amesema “Huo ndio utakaso unaozungumziwa. Unataka kuliondoa kundi moja na kuliacha jingine unalopendelea. Lakini kitu kingine ni kwamba FDLR na makundi mengine unayoyasikia yanafanya hizi kelele zote. Kuna watu wanadhani kwamba wanajaribu kutafuta mbinu mbadala tofauti na ilivyo Rwanda.”
Kundi hilo la FDLR, linajumuisha waliokuwa wanajeshi wa serikali ya Rwanda, (iliyokuwa madarakani kabla ya kupinduliwa na waasi wa RPF lililoongozwa na rais Paul Kagame, mwaka 1994), na wengi wao ni kutoka kabila la wahutu wanashutumiwa kwa kusababisha mauaji ya Watutsi Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.