Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge ameonyesha kuchukizwa na kitendo cha kusuasua kwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kinondoni Studio kuelekea Mwananyamala yenye urefu wa Km 4.2, jambo linalopelekea usumbufu kwa wananchi hususani wagonjwa wanaokwenda kupata huduma Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala.
Kutokana na hilo RC Kunenge amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kutoka Kampuni ya CRSG kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili ifikapo Julai 30 barabara iwe imekamilika kwa 100% na kuahidi kuwa ndani ya Mwezi mmoja kuanzia leo atarudi kukagua maendeleo ya Ujenzi.
Aidha, Kunenge amewaonya TARURA kutokumuongezea muda Mkandarasi huyo na kuwaelekeza kuwa wakali na kusimamia kikamilifu mradi huo.
Kunenge ameeleza kuwa miongoni mwa mambo yaliyomkwaza zaidi ni kuona hadi kufikia sasa muda wa mradi umefikia 62% huku kazi iliyofanyika ni ikiwa ni 16% pekee, wahusika wakitoa sababu dhaifu.
Kwa upande wake Makamu Mhandisi Mshauri wa Mradi huo kutoka Kampuni ya HP Gauf, Wile John amemuahidi Mkuu wa Mkoa kuwa maagizo aliyotoa watayatekeleza kwa wakati.
Ujenzi wa Barabara ya Kinondoni Studio kuelekea Mwananyamala yenye urefu wa kilometa 4.2 unatekelezwa na Mkandarasi kutoka kampuni ya CRSG.