Kundi la wafanyakazi wanaotoa huduma za kibinadamu chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), linaingia nchini leo, Mei 15, 2020 kwa ndege ya shirika hilo kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Ndege hiyo kutoka Addis Ababa nchini Ethiopia itakuwa ya kwanza kutua baada ya Serikali kuzuia safari za ndege za abiria kuingia au kutoka nchini, ikiwa ni hatua za awali za kukabiliana na maambukizi ya virusi vipya vya corona (covid-19).
Safari za ndege hiyo ni sehemu ya mpango wa Shirika la Umoja wa Mataifa la UNFPA kutoa msaada duniani wakati mapambano dhidi ya covid-19 yakiendelea.
Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania, Michael Dunford amesema kupitia taarifa yake kuwa huduma inayotolewa na shirika hilo ni kuhakikisha wanatoa msaada unaotakiwa kwa watu wenye mahitaji maalum ili kuwasaidia kupambana na mlipuko wa virusi hivyo.
“Kama Wakala wa Umoja wa Mataifa unaoongoza katika kutoa misaada na mpangilio, itahakikisha kuwa misaada ya kibinadamu na wafanyakazi husika wanafika katika maeneo yote yenye uhitaji duniani,” amesema Dunford.
WFP wameeleza kuwa wafanyakazi wanaoingia leo watafuata masharti ya Serikali ya kukaa karantini kwa siku 14 ili kuangalia kama wana maambukizi ya virusi vya corona.
Kim Jong Un ashtukia usalama? Awatumbua Mkuu wa Intelijensia na wa Ulinzi wake