Meneja wa Arsenal Mikel Arteta amejitosa kwenye vita ya kumuwania beki wa kushoto wa Paris Saint-Germain, Layvin Kurzawa, ambaye atapatikana bure kwenye dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi.
Arteta amejitosa kwenye vita hiyo, huku akifahamu wazi matajiri wa jijini London Chelsea nao wapo kwenye kwenye mchakamchaka wa kufukuzia huduma ya beki huyo kutoka Ufaransa.
Arsenal ipo sokoni kunasa wachezaji wa gharama nafuu baada ya bajeti yao ya usajili kubana kutokana na janga la corona. Chelsea wao wamekuwa wakimtolea macho Kurzawa, wakiamini ni chaguo mbadala kwenye mpango wao wa kunasa huduma ya Ben Chilwell kama watashindwa kumsajili kutoka Leicester City.
Kocha wa Leicester City, Brendan Rodgers anaamini watabaki na huduma ya beki wao huyo wa kushoto kwenye dirisha la mwaka huu la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Marcos Alonso na Emerson wameshindwa kufanya mambo na kumfanya Frank Lampard kumwambia mkurugenzi anayeshughulikia mambo ya usajili huko Stamford Bridge, Marina Granovskaia kumletea mabeki wapya wa pembeni.
Kurzawa, aliwahi kuichezea Monaco yupo kwenye kikosi cha PSG tangu msimu wa 2015/16, akicheza jumla ya mechi 123 kwenye kikosi hicho na kubeba mataji matatu ya Ligue 1, matatu ya Kombe la Ufaransa na mengine kibao, huku mkataba wake ukimalizika mwisho wa msimu.