Uongozi wa Uwanja wa Taifa umewataka mashabiki wanaofika uwanjani hapo kuendelea kuzingatia taratibu za wataalamu wa afya, ili kuepuka maambukizi ya virusi vya Corona.

Ombi hilo kwa mashabiki wa soka wanaofika uwanjani hapo kuzishangilia timu yao, limetolewa ili kuuepusha uwanja huo mkubwa kuliko viwanja vyote nchini, kukwepa adhabu ya kutumika bila uwepo wa mashabiki kama ilivyotokea kwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Meneja wa Uwanja wa Taifa, Nsajigwa Gordon amesema mashabiki walioingia katika uwanja wa Taifa tangu ligi iliporejea wamejitahidi kufuata taratibu ambazo zimewekwa na mamlaka za serikali.

Amesema hata katika mchezo uliopita kati ya Young Africans dhidi ya Azam FC mashabiki walifuata taratibu, hivyo wao kama wasimamizi wa uwanja wanajisikia faraja kuona taratibu zinafuatwa.

“Kwa kweli mashabiki Taifa wanafuata taratibu za wataalamu wa afya na waendelee na utaratibu huo huo kama ambavyo wamefanya katika mechi zilizopita,” alisema Gordon.

Anasema tayari wameshaona mfano kwa uwanja wa Jamhuri kufungiwa hivyo ni vyema kufuata taratibu ili wasikumbwe na adhabu ambayo wenzao wamekutana nayo.

Aidha Gordon anasema wako makini katika kutekeleza maelekezo ya wataalamu wa afya katika kukabiliana na virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid19.

Juma lilolopita Serikali iliipa adhabu timu ya JKT Tanzania kucheza michezo yake ya nyumbani kwenye uwanja wa Jamhuri bila uwepo wa mashabiki baada ya kushindwa kuzingatiwa taratibu za wataalamu wa afya za kukabiliana na virusi vya Corona, katika mchezo uliowakutanisha dhidi ya young Africans na timu hizo kutoka sare ya bao moja kwa moja.

Kurzawa kuzigonganisha Arsenal, Chelsea
TAKUKURU yawatia mbaroni wafanyakazi 30 wa MSD