Mabingwa wa Kombe La Shirikisho Tanzania bara (ASFC) Azam FC wamewasili mjini Bukoba, tayari kwa mchezo wa mzunguuko wa 31 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar.

Mchezo huo utachezwa kesho Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, huku Azam FC wakiwa na mipango mizuri ya kuendelea kubaki katika nafasi ya pili kwa kuzidisha alama zao 58, nyuma na Simba SC walio kileleni kwa kumiliki alama 75.

Kagera Sugar ambayo pia imeshacheza michezo 30 inashika nafasi ya 9 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kumiliki alama 41.

Kikosi cha Azam FC kiliondoka Dar es salaam mapema asubuhi ya leo, mishale ya saa tatu asubuhi kiliwasili mjini Bukoba, na jioni kitafanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa Kaitaba.

Mkuu wa idara ya habari na mawasilino ya Azam FC Thabit Zakaria (Zaka Zakazi) amesema kwa hakika safari yao ya kuelekea mjini humo imekua nzuri na wamefika kwa wakati walioukusudia.

“Tumesafiri na wachezaji 22, asilimia kubwa ya wachezaji waliocheza mchezo dhidi ya Young Africans tumesafiri nao, tuna imani wataendelea kupambana na kuapata matokeo mazuri.” Amesema Zaka Zakazi baada ya kuwasili mjini Bukoba.

Kikosi kilichosafiri hadi mjini Bukoba yupo Benedict Haule, Mwadini Ally, Abdul Hamahama, Nicholaus Wadada, Oscar Masai, Abdallah Heri Sebo, Aggrey Moris, Lusajo Mwaikenda, Salmin Hoza na Bruce Kangwa.

Wengine ni Idd Nado, Iddi Kipawile, Frank Domayo, Brayson Raphael, Mudathir Yahya, Never Tigere, Obrey Chirwa, Khlefin Hamdou ‘Finito’, Richard Djodi, Andrew Simchimba, Shabani Idd Chilunda, Abdallah Masoud na Cabaye.

Azam FC iliyo chini ya Aristica Cioaba,itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kulazimisha sare ya bila kufungana na Young Africans Uwanja wa Taifa, mwishoni mwa juma lililopita.

Kwa upande wa wenyeji Kagera Sugar watashuka uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC Uwanja wa Majaliwa, mkoani Lindi mwishoni mwa juma lililopita.

TPLB kuijadili Azam FC
Mourinho azungumzia tuhuma za kuua vipaji