Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kauli ya Serikali ya kuthamini shughuli za kilimo na ufugaji nchini haimaanishi kuwa wafugaji wanaruhusiwa kuingiza mifugo na kulisha kwenye mashamba ya wakulima, wala wakulima kudhuru mifugo ya wafugaji.
Mjaliwa ametoa kauli hiyo na kuzisisitiza pande hizo mbili kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu, kwani tayari Serikali imeshaandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo ya makazi, huduma za kijamii, kilimo na mifugo hivyo hakuna mwenye haki ya kumvamia mwingine.
Amesema, Watendaji wa vijiji wanatakiwa kuhakikisha kabla ya kuwakaribisha wafugaji katika maeneo yao wajiridhishe kama wana maeneo ya kutosha kwa ajili ya shughuli hiyo na pia wawashirikishe wanakijiji husika juu ya ujio wa wafugaji na wafahamu idadi ya mifugo waliyonayo.
Aidha, Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi hao waendelee na shughuli zao za kilimo na wasiogopewa kwani Serikali ipo makini na inaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote nchini vikiwemo na vijiji vyao. Wananchi hao walimuelezwa kuwa wanaogopa kuendelea na maandalizi ya mashamba kutokana na kuhofia uvamizi wa mifugo.