Uongozi wa Young Africans umetoa ufafanuzi kwa nini haukuwaaga kwa heshima wachezaji Mrisho Ngassa, Juma Abdul na Kelvin Yondani, kama walivyofanya kwa kiungo kutoka Rwanda Haruna Niyonzima.
Young Africans walitumia muda wao baada ya mchezo dhidi ya Ihefu FC juzi Alhamis (Julai 15), kumuaga kwa heshima Niyonzima mbele ya Mashabiki na Wanachama waliojitokeza Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam.
Kitendo hicho kiliibua maswali mengi kwa wadau wa Soka Tanzania, kwa kuhoji kwa nini iwe kwa Niyonzima na sio wachezaji wengine ambao walipambana na kuondoshwa kimya kimya?
Mkuu wa Idara ya Habari ya Young Africans Hassan Bumbuli amesema, Uongozi ulitafakari kwa kina kabla ya kufanya tukio hilo na ulibaini kuna haja ya kumuaga Niyonzima kwa heshima tofauti na wengine walioondoka.
“Niyonzima amefanya makubwa ndani ya timu na mchango wake umeonekana na anaondoka kwa amani, ndio maana hata sisi tumethamini kile alichokifanya,” amesema na kuongeza:
“Hawa wachezaji wetu (Ngassa, Juma Abadul na Yondani) waliondoka vibaya, kwanza klabu ilikuwa bado inawahitaji na tulitaka kuwaongezea mikataba, lakini hawakuwa tayari basi tukawaacha wakafanye maisha mengine.”
Haruna Niyonzima anaondoka Young Africans baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa miaka minane, kwa mafanikio ya kutwaa mataji ya Tanzania Bara zaidi ya mara tatu, Kombe la Shirikisho (ASFC) mara moja na kuifikisha timu hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili.