Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amekiri kuwa katika harakati za kumfuatilia mshambuliaji kinda wa klabu ya AS Monaco Kylian Mbappe.
Wenger amethibitisha taarifa hizo, kwa kunadi hadharani kuwa anaamini Mbappe huenda akawa Thierry Henry mpya.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 18, aalianza kucheza ligi ya nchini Ufaransa (Ligue 1) akiwa na miaka 16 na mpaka sasa ameshafunga mabao 6 katika michezo 19.
Mbappe, ambaye ni sehemu ya wachezaji wanaounda kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa chini ya umri wa miaka 19, ameweka historia ya kuwa mfungaji bora wa Ligue 1 mwenye umri mdogo.
“Sisemi kama anafanana kila kitu na Thierry Henry, lakini ukweli ni kwamba, kuna baadhi ya vitu wanashabihiana hususan katika umiliki wa mpira na ufungaji,” Alisema Wenger alipohojiwa kwenye kipindi cha Ligue 1 show.
“Hapa ninazungumzia kufanana kwao, naamini kwa siku kadhaa zijazo ataendelea kukaribia viwango vya Henry au hata kumpita.
“Tunamfuatilia, Tunamfahamu vizuri sana, naamini kama tutafanikiwa kumpata tutamuendeleza kwa mambo mengi zaidi. Msimu uliopita alisaini mkataba mpya na klabu ya AS Monaco ambapo naamini utaamua mustakabali wake.”