Gwiji wa klabu ya Arsenal Robert Pires, amesema nafasi ya mwisho ya ubingwa wa England kwa klabu hiyo msimu huu, ipo mikononi mwa Chelsea.

Pires ambaye kwa sasa ni sehemu ya benchi la ufundi la Arsenal, anaamini mchezo wa kesho wa mahasimu hao wa jijini London, utatoa picha kamili kwa The Guneers kama wataendelea kuwepo katika mbio za ubingwa ama la.

Pires amebainisha jambo hilo alipohojiwa katika kipindi cha Sky Sports News HQ kinachorushwa na televisheni ya Sky Sports kila siku asubuhi.

Amesema baada ya Arsenal kupoteza mchezo dhidi ya Watford kwa kufungwa mabao mawili kwa moja, watakua na nafasi adhimu ya kuendelea kuwa katika harakati za kuufukuzia ubingwa msimu huu, endapo watagangamala mbele ya Chelsea na kupata matokeo mazuri.

Hata hivyo amekiri mchezo wa kesho dhidi ya Chelsea hautokua rahisi kwa The Gunners kutokana na kikosi cha Antonio Conte kuhitaji kuendeleza kasumba ya ushindi kama walivyofanya katika mapambano mengine kabla ya kukutana na Liverpool mwanzoni mwa juma hili, ambapo waliwalazimisha matokeo sare.

Jambo lingine ambalo linamuamunisha Pires kuhusu ugumu wa mchezo wa kesho, ni hatua ya Chelsea ya kutaka kulipa kisasi cha kufungwa na Arsenal mabao matatu kwa sifuri kwenye mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa ligi ya England uliochezwa Emirates Stadium.

Lakini pamoja na kueleza mambo hayo, bado Pires amesisitiza Arsenal wamejiandaa vizuri kuelekea katika mpambano wa kesho utakaochezwa Stamford Bridge.

Kwa sasa Arsenal wanashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ya nchini England wakiwa na point 47, huku Chelsea wakiongoza msimamo huo kwa kufikisha point 56.

Makamba afungua mkutano wa tathmini ya athari za mazingira
Kylian Mbappe Amvutia Arsene Wenger