Wataalamu wa Tathmini ya Athari za Mazingira nchini wametahadharishwa kuwepo kwa matapeli wanaoingilia taaluma hiyo kwa lengo la kufanya udanganyifu na kujipatia kipato.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira January Makamba, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Tathmini ya Athari za Mazingira Tanzania (TEEA) leo Jijini Dar es Saalam.

Makamba amesema kuwa taaluma ya tathmini ya Athari za Mazingira ni ya shughuli ambayo inahitaji umakini mkubwa sana na ni kwa mujibu wa sheria za nchi lakini kumekuwapo na makanjanja ambao wamekuwa wakifanya uraghai kwa wawekezaji na kutia doa tasnia nzima ya taaluma ya uthamini wa athari za mazingira.

“Serikali inakusudia kubadilisha kanuni na taratibu ili kuongeza udhibiti wa udanganyifu katika eneo la Tathmini ya Athari za Mazingira(IAE) kwa kuweka viwango stahiki kwa wataalamu wa tathmini ya athari za mazingira vitakavyozingatia elimu na uzoefu,” amesema Makamba.

Aidha, Makamba amesema kuwa ni vyema sasa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Chama cha Wataalumu hao kushirikiana  kuhakikisha taaluma hiyo haingiliwi na makanjanja ili kufanikisha utoaji wa huduma zenye viwango stahiki na vya kuridhisha.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mhandisi Bonaventure Baya amesema kuwa mkutano huo umekuwa ukiwakutanisha Wataalamu wa Tathmini ya Athari za Mazingira nchini ambapo utumia fursa hiyo kukumbushana mambo yanayohusu weledi na majukumu yao.

Video: Vanessa,Tunda, Polisi 3 watajwa madawa ya kulevya
Robert Pires: Silaha Ya Mwisho Ya Arsenal Ipo Kwa Chelsea