Matajiri wa mjini Paris nchini Ufaransa Paris Saint-Germain (PSG) wameafiki dili la kumsajili kwa mkopo mshambuliji kinda Kylian Mbappe kutoka kwa mahasimu wao AS Monaco.
Kinda huyo anatarajiwa kuondoka AS Monaco kwa mkopo wa mwaka mmoja, utakaogharimu kiasi cha Euro milioni 166.
Mbappe mwenye umri wa miaka 18 aliachwa kwenye benchi wakati wa mchezo wa ligi ya nchini Ufaransa hapo jana dhidi ya Olympic Marseille, waliokubali kichapo cha mabao sita kwa moja, hali ambayo iliendelea kudhihirisha uhakika wa mshambuliaji huyo kuondoka klabuni hapo.
Mshambuliaji huyo wa kifaransa, amecheza mchezo mmoja tangu msimu wa 2017/18 ulipoanza, na sababu kubwa iliyomzuia kutokua sehemu ya kikosi katika michezo miwili iliyopita kabla ya ule wa jana, iliripotiwa kuwa anamaumivu ya goti yaliyokua yanamkabili.
Mbappe amekua akihusishwa na mpango wa kuondoka Stade Louis II tangu mwishoni mwa msimu uliopita, na klabu kadhaa ikiwepo Real Madrid, Manchester United, Manchester City, Arsenal na FC Barcelona zilitajwa kuwa katika mawindo ya kumuwania.
Hata hivyo taarifa za awali zinaeleza kuwa, ushawishi mkubwa wa usajili wa Mbappe kuelekea mjini Paris, umechagizwa na uwepo wa mshambuliaji kutoka nchini Brazil Neymar aliyesajiliwa mapema mwezi huu, akitokea FC Barcelona kwa ada iliyoweka rekodi duniani.
Wakati huo huo AS Monaco wameanza kujipanga kuziba pengo litakaloachwa wazi na Mbappe, kwa kumfikiria mshambuliaji kutoka nchini Montenegro na klabu ya Inter Milan ya Italia Stevan Jovetic.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, alipelekwa kwa mkopo Sevilla CF msimu uliopita, baada ya kuwa na mazingira magumu ya kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Inter Milan.