Nguvu ya mitandao ya kijamii katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja imeendelea kudhihirika baada ya mrembo Kylie Jenner, kuitumia mitandao ya kijamii kufanikisha biashara yake ya vipodozi iliyompa ubilionea akiwa mdogo.
Forbes limemtangaza Kylie mwenye umri wa miaka 21 kuwa amevunja rekodi ya kuwa mtu aliyewahi kuwa bilionea akiwa na umri mdogo zaidi, akiipiku rekodi iliyowekwa na mmiliki wa Facebook, Mark Zuckerberg aliyekuwa bilionea akiwa na umri wa miaka 23.
“Nilipoanza sikutegemea kitu chochote kikubwa, nilipenda tu kuanza kuuza vipodozi kwa mapenzi kwa mashabiki wangu,” Forbes linamkariri Kylie.
“Ni nguvu ya mitandao ya kijamii ndiyo iliyofanikisha, nikafikia umbali huu hata kabla sijawa na uwezo wa kuanza lolote,” ameongeza.
Kylie ana wafuasi zaidi ya Milioni 128.6 kwenye Instagram pekee, yaani zaidi ya mara mbili ya idadi ya watu nchini.
Kylie alianza kuuza vipodozi vyake kwa kutumia mitandao ya kijamii miaka mitatu iliyopita, akiuza kikopo kimoja cha lipstick kwa $29 (Sh. 68,500 za Kitanzania).
Lakini kwa nguvu ya mitandao hiyo, alipata umaarufu na kuanza kufungua maduka na usambazaji ambapo mwaka jana biashara yake ilikadiriwa kuwa na thamani ya $360 milioni. Lakini mwaka huu, biashara hiyo imethaminishwa na Forbes kuwa ni $900 milioni na inamilikiwa na mrembo huyo kwa 100%.
Kufuati hatua hiyo, Forbes wameeleza kuwa kwa kuzingatia kiasi cha fedha anazomiliki kutokana na mambo mengine kama kushiriki kwenye mitindo ya mavazi, kuonekana kwenye kipindi cha familia yake cha ‘Keeping Up with the Kardashians’, amefikia utajiri wa $1 bilioni.
Kylie ni mtoto wa mwisho kwa Kris Jenner (mama), akiwa na dada yake Kendal Jenner kupitia kwa baba yao Bruce Jenner. Lakini pia ana dada zake ambao sio wa baba mmoja lakini ni wa mama mmoja, ‘The Kardashians’. Hivyo, kwa upande huo ni mdogo wake wake Kim, Khloe, Kourtney na Rob.