Msanii wa Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo maarufu kama ‘Lady Jaydee’ ametaka kujiua kwa kisa ambacho hakijawekwa wazi.

Lady Jay Dee amedai kuwa siku ya jana alitamani kunywa sumu ila nafsi yake ilimsuta na kukumbuka alipotoka jambo lililomfanya aone kujiua ni ujinga.

Jide ambaye anajiandaa na onyesho lake la Usiku wa Sauti (Vocal Night) litakalofanyika Oktoba 26 mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, alitumia ukurasa wake wa ‘Twitter’ kuandika ujumbe huo uliotikisa tasnia ya burudani.

“Jana (juzi) nilihisi kunywa sumu ila kabla sijafanya nikajisuta na kujikumbusha nilipotoka na kujiuliza nitakuwa mjinga kiasi gani. Nikajisikitikia tu kisha nikaacha na leo bado nipo kigumu gumu ila bado nipo,” ameandika Jide.

Kulingana na wanasaikolojia wa afya wamefanyia uchunguzi tatizo linalopelekea watu wengi kufikia hatua ya kukata tamaa na kujiua na kugundua kuwa hali hii inaletwa na ugonjwa unaofahamika kama Sonona (Depression) ni hali ya kujisikia huzuni iliyopitiliza na kupoteza hamu ya kufanya shughuli ambazo mtu ulikuwa ukifurahia kuzifanya ikiambatana na kushindwa kufanya kazi zako za kila siku kwa muda wa wiki mbili(2).

Takwimu za dunia zinaonesha kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaoathiriwa na Sonona ambapo takribani watu milioni 322 duniani wanaishi na hali hii, Sonona huwaathiri sana wanawake(5.1%) kuliko wanaume(3.6%).

Hata hivyo wanasaikolojia wamebainisha kuwa kibailojia ugonjwa huu unasababishwa na Kushindwa kukabiliana na changamoto za kijamii zinapotokea, mtazamo hasi wa mambo yanayotokea kila siku katika maisha, Upweke pamoja na Kunyanyaswa kihisi au kijinsia katika maisha ya kila siku au enzi za ukuaji.

Lakini pia zipo sababu za kijamii kama vile matokeo mabaya kwa mambo ambayo tulitaraji vizuri, kufeli mitihani, kushindwa kufikisha malengo, matatizo au migororo katika familia au mahusiano, kukosa ajira, kupoteza mali mbalimbali kama pesa, samani, umasikini uliokithiri, Kuwa tegemezi, Kukosa huduma mbalimbali za kijamii, Kuugua kwa muda mrefu na kadhalika.

Hivyo mara nyingi athari kubwa inayoweza kusababishwa na ugonjwa huu ni pamoja na mtu kuchukua hatua ya kujiua, na takwimu zimeonesha kuwa kujiua imeonekana kuwa sababu ya pili duniani inayopelekea vifo vya vijana wengi.

 

Wanusurika kifo baada ya Ndege kudondoka baharini
Madaktari walipishwa bilioni 70 kwa uzembe wa kumtahiri mtoto wa siku 18