Beki kisiki wa Young Africans Lamine Moro amepona majeraha yaliyomuweka nje kwa wiki kadhaa na yuko tayari kuitumikia timu hiyo kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya JKT Tanzania hapo kesho.
Moro aliumia katika mchezo wa mtoano kombe la Shirikisho dhidi ya Pyramids FC uliopigwa nchini Misri mapema mwezi huu, na Young Africans walikubali kufungwa mabao matatu kwa sifuri.
Moro pamoja na Ally Ally wote walishindwa kumaliza mchezo huo ambao Young Africans ililazimika kucheza na wachezaji 10 baada ya kuwa imemaliza ‘sub’ zote.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu ya Young Africans, Hassan Bumbuli amesema mabeki hao wote wamepona sambamba na Mohammed Issa ‘Banka’ ambaye pia alikua anasumbuliwa na majeraha.
Bumbuli amesema kama ikimpendeza Kaimu Kocha Mkuu Charles Mkwasa, anaweza kuwatumia wachezjai hao kwenye mchezo wa kesho dhidi ya JKT Tanzania, ambao utaunguruma uwanja wa Uhuru, jijini Dar es salaam kuanzia mishale ya saa kumi jioni.
Hata hivyo bubuli aliwataja wachezajia mbao bado ni majeruhi na wanaendele na matibabu ni Paul godfrey “Boxer” na Juma Mahadhi.
Wakati huo huo mshambuliaji kinda Maybin Kalengo amerejea kwao kuuguza majeraha baada ya kufanyiwa upasuaji kufuatia kuvunjika mguu jijini Mwanza.
Kalengo aliumia kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Pamba FC, alifanyiwa upasuaji Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es salaam.
Inaelezwa uongozi wa Young Africans umempa ruhusu arudi kwao wakati akiendelea kupona majeraha hayo yatakayomuweka nje kwa miezi mitatu.
Wakati Kalengo akipewa ruhusa hiyo, kiungo mshambuliaji Issa Bigirimana nae ameomba ruhusu arejee kwao akatibiwe majeraha yanayomsumbua mara kwa mara.
Bigirimana hajawa na mwanzo mzuri kwenye kikosi cha Young Africans, kwani tangu asajiliwe hajacheza mchezo wowote wa mashindano, kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.