Benjamin Netanyahu, amekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Israel aliyeko madarakani kufunguliwa mashtaka ya rushwa, udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka (kupoteza imani).

Mwanasheria mkuu wa Israel ametangaza hatua hiyo leo, Novemba 21, 2019 akieleza kuwa Netanyahu atachunguzwa kwa tuhuma hizo pamoja na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka dhidi yake.

Katika mashtaka hayo, waziri mkuu huyo anadaiwa kupokea zawadi za thamani kubwa kutoka kwa wafanyabiashara kwa lengo la kuwasaidia akitegemea kupewa nafasi chanya kwenye tovuti ya wafanyabiashara hao.

Hata hivyo, Netanyahu ambaye ametumikia nafasi ya uwaziri mkuu wa Israel kwa kipindi cha miaka 13 alikana mashataka hayo na kueleza kuwa yanatengenezwa na wapinzani wake kisiasa kwa lengo la kumshinikiza kujiuzulu.

Amesema hatajiuzulu nafasi hiyo kama ambavyo wengi wamekuwa wakisubiri achukue hatua hiyo.

Rais wa Israel, Reuven Rivlin ameliambia Bunge la nchi hiyo kujadili nafasi ya uwaziri mkuu ndani ya kipindi cha siku 21. Mpinzani mkuu wa Netanyahu, Benny Gantz amesema anajiandaa kuunda Serikali ya mseto.

Sakata la tuhuma dhidi ya Netanyahu zilishika kasi Februari mwaka huu baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kueleza kuwa amepanga kufungua mashtaka dhidi yake. Aliyataja mashtaka hayo kwa makundi matatu, akiyapa majina ya ‘Case 1,000’, ‘Case 2,000 na Case 4,000.

Mashtaka mazito zaidi yako katika ‘case 4,000’ ambayo inahusu rushwa, udanganyifu na kupoteza imani.

Kwa maelezo ya case 4,000: inaelezwa kuwa Netanyahu alitumia ofisi yake vibaya na kufanya uamuzi ambao unapendelea kampuni kubwa zaidi ya mawasiliano ya simu nchini humo ili aweze kupata nafasi ya kuwekwa kwenye taarifa za habari kwenye tovuti yao maarufu, kama sehemu ya makubaliano na wanahisa wa kampuni hiyo.

Hata hivyo, Netanyahu amekanusha vikali tuhuma hizo akieleza kuwa maamuzi yalifikiwa baada ya wataalam kumshauri na kwamba hakupata chochote kama shukurani ya uamuzi huo.

Arusha: Mkutano wa 39 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki waanza
Lamine Moro, Ally Ally, Banka kuikabili JKT Tanzania