Beki na Nahodha wa Young Africans Lamine Moro amerejeshwa kambini, baada ya benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Nabi kukutana na Uongozi na kukubalina mchezaji huyo arudishwe kikosini.
Lamine Moro alisimamishwa kwa utovu wa nidhamu na hakuwa sehemu ya kikosi cha Young Africans kwa kipindi kirefu, jambo ambalo lilizua taharuki kwa Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo.
Mkuu wa Idara ya Habari ya Young Africans Hassan Bumbuli amethibitisha taarifa za kurejea kwa beki huyo, ambaye aliwahi kuhusishwa kutaka kuondoka klabuni hapo kufuatia kuchoshwa na taarifa za utovu wa nidhamu ambao haukutolewa ufafanuzi kamili na uongozi.
Bumbuli amesema baada ya mazungumzo yalimuhusisha mchezaji, uongozi na benchi la ufundi , Lamine amelazimika kurudi kambini kuendelea na maandalizi ya michezo miwili ya mwisho ya Ligi Kuu pamoja na mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho.
Lamine Moro alionekana kwa mara ya kwanza akiwa na wachezaji wa Young Africans, juzi Jumamosi (Julai 10), wakati wa hafla maalum iliyoandaliwa na Mfadhili wa klabu hiyo GSM, kwa kutoa pongezi kufuatia ushindi dhidi ya Simba SC uliopatikana Julai 03, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Wakati huo huo, suala la Mlinda Lango Metacha Mnata bado lipo mikononi mwa Uongozi na hajaruhusiwa kuingia kambini kwa sababu anaitumikia adhabu ya TFF.