Mabingwa wa kihistoria katika Soka la Bongo ‘Young Africans’ wametamba kuzinyakua alama sita za michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyobaki, ili kujiimarisha katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Young Africans iliyokusanya alama 70 baada ya kucheza michezo 32, imebakiza michezo miwili dhidi ya Ihefu FC utakaochezwa Alhamisi (Julai 15) na Dodoma Jiji FC utakaochezwa mwishoni mwa juma hili.

Mkuu wa Idara ya Habari ya Young Africans Hassan Bumbuli amesema wamejipanga kupambana katika michezo hiyo, ili kufikia lengo la kupata alama sita ambazo zitawawezesha kumaliza Ligi Kuu msimu huu 2020/21, wakiwa na alama 76.

Bumbuli amesema kwa namna ambavyo wamejipanga wana uhakika wa kupata alama zote sita ambazo watazipambania dhidi ya Ihefu FC na Dodoma Jiji FC.

“Nikuhakikishie kwamba mechi zetu mbili ambazo zimebaki hapo tuna uhakika wa kuchukua pointi zote sita hii yote inatokana na maandalizi mazuri ambayo tumefanya.”

“Kikubwa ni kuona kwamba kwenye kila mechi tunafanya vizuri na hilo lipo wazi ukizingatia kwamba kila mchezaji anatimiza majukumu yake anayopewa,” amesema Bumbuli.

Ikiwa Young Africans itafanikiwa kuzifunga Ihefu FC na Dodoma Jiji FC itafikisha jumla ya alama 76, nyuma ya Mabingwa wa Simba SC ambao kwa sasa wana alama 79, baada ya kuifunga Coastal Union mabao 2-0 jana Jumapili (Julai 11) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Lamine Moro mambo safi Young Africans
Dube kuikosa Simba SC?