Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Didier Gomes ametuma ujumbe kwa timu zitakazocheza na kikosi chake kabla ya kumaliza msimu huu 2020/21.

Gomes ametuma ujumbe huo, baada ya kuikishuhudia kikosi chake kikitawazwa kuwa Mabingwa mara nne wa Ligi Kuu Tanzania Bara jana Jumapili (Julai 11), baada ya kuifunga Coastal Union, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa amesema atahakikisha kikosi chake kinaendelea kufanya vizuri katika michezo ya Ligi Kuu iliosalia na Kombe la Shirikisho ikiwa ni sehemu ya malengo waliojiwekea msimu huu 2020/21.

Katika Ligi Kuu Simba SC imekusanya alama 79 ikiwa nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi hiyo, huku ikibakiza michezo miwili dhidi ya Azam FC na Namungo FC.

Pia wana kazi ya kucheza na watani zao wa jadi kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho itakuwa ni Julai 25 watakapokutana na Young Africans, Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

“Hatujawa kwenye furaha kubwa hasa ukizingatia tumetoka kupoteza mbele ya Young Africans ila ni suala la matokeo. Ambacho kimebaki kwa sasa ni kuona kwamba mechi zetu zote kuanzia hizi za ligi mpaka ile ya fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Young Africans tunashinda.”

“Tulibainisha tangu awali kwamba tunahitaji kushinda mechi zote, kushinda mataji yote hivyo jambo pekee ambalo tunalo kwa sasa ni kuendelea kushinda kwenye mechi zetu zote.”

“Kupoteza mchezo uliopita haina maana kwamba hatuna ubora hapana lakini tuna kazi ya kufanya na mashabiki waendelee kutupa sapoti,” amesema Gomes.

Simba SC itakua mgeni wa Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi keshokutwa Jumatano (Julai 14), na itamaliza msimu huu kwa kupapatuana dhidi ya Namungo FC, Julai 18, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Dube kuikosa Simba SC?
PICHA: Serikali yakagua mkongo wa taifa bandari ya Mtwara