Meneja wa klabu ya Chelsea Frank James Lampard anaendelea kuwa na wakati mgumu, kufuatia matokeo mabaya yanayokikabili kikosi chake kwenye michezo ya Ligi Kuu ya England.
Lampard alikishuhudia kikosi chake usiku wa kuamkia leo, kikifungwa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Leicester City waliokua nyumbani King Power Stadium, na kufiksha idadi ya michezo sita waliyopoteza msimu huu 2020/21.
Kupoteza alama tatu za mchezo dhidi ya Leicester City, kunakiweka rehani kibarua cha meneja huyo, ambaye aliwahi kuitumikia Chelsea kama mchezaji kuanzia mwaka 2001 hadi 2014.
Fedha za usajili zilizotumiwa na Lampard wakati wa usajili wa majira ya kiangazi nazo zinaongeza uzito wa kupoteza kibarua chake, endapo ataendelea kupoteza alama kwenye michezo ya Ligi Kuu ya England.
Baada ya mchezo wa jana dhidi ya Leicester City, waandishi wa habari walimuuliza Lampard kuhusu mustakabali wake ndani ya Chelsea, ambapo alijibu kwa kusema: “Sina uwezo wa kuamua hilo. Nimekuwa nikiulizwa hili swali kwa wiki kadhaa sasa. Ninaelewa ni kwa nini, ni matarajio ya klabu kama ni sawa au sio sawa.”
“Niliichukua hii kazi nikijua kutakuwa na kipindi kigumu kutokana na kuwa na timu ambayo haipo tayari kwa mashindano. Tulifungiwa (kusajili), tunawachezaji wadogo, tumesajili wachezaji wapya ambao tunaona wanajitahidi kuzoea mazingira.
“Tunachoweza kukifanya kwa sasa ni kuendelea kupambana.”
Chelsea inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi kuu ya England, baada ya kucheza michezo 19, huku ikikusanya alama 29 zilizotokana na michezo minane walioshinda, wamepoteza michezo sita na kutoka sare michezo mitano.