Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza Afisa Elimu wa Wilaya ya Ruangwa anayeshughulikia elimu ya msingi, Selemani Mrope atafute walimu wawili kutoka Ruangwa na kuwahamishia kata ya Nanganga mara moja.
Ametoa agizo hilo jana Jumamosi, Julai 27, 2019) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nanganga, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi alipopita kuwasalimia wakazi hao.
Waziri Mkuu alipokea taarifa ya shule ya msingi Nanganga ambayo ilionyesha kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 237 ina walimu sita tu. kati ya hao, wavulana ni 124 na wasichana ni 113.
“Lazima kuna walimu wamejazana pale Ruangwa mjini, nenda kaandike barua za uhamisho Jumapili, wahusika wapewe barua zao na Jumatatu waje kuripoti hapa Nanganga,” amesema Waziri Mkuu na kuamsha shangwe miongoni mwa wakazi wa Nanganga.
Waziri Mkuu ambaye amewasili Lindi kwa mapumziko mafupi, alipokea taarifa ya shule ya msingi Nanganga ambayo ilionyesha kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 237 ina walimu sita tu. kati ya hao, wavulana ni 124 na wasichana ni 113.
“Shule hii ina madarasa nane likiwemo darasa la awali, masomo yanayofundishwa ni tisa, mkibaki na walimu hawa sita, mzigo unakuwa mkubwa kwa walimu hawa waliopo. Afisa Elimu tafuta wawili walimu waje hapa Jumatatu, na Mkurugenzi wa Halmashauri atakupa gari ya kuwahamishia hapa,” ameongeza Waziri mkuu.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa Ruangwa, amewataka wakazi wa kata hiyo wafikirie kuanza ujenzi wa shule ya sekondari yao ya kata ili kuwapunguzia safari wanafunzi wa kijiji hicho ambao kwasasa wanalazimika kwenda kusoma Nangumbu, iliyoko umbali wa km. 10.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Serikali imetoa shil. milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne ambayo yakikamilika walimu watapata ofisi pia.
Pia amemwambia diwani wa kata ya Chinongwe, Maki Camillius kwamba katika bajeti ya mwaka huu, kata hiyo itapatiwa shil. milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nne za walimu katika shule ya sekondari ya kata ya Chinongwe.
Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Amiri Musa Kambona amesema kuwa madarasa mawili na ofisi moja ya walimu vilibomoka mwaka 2014 kutokana na mvua na upepo mkali na kusababisha upungufu wa madarsa na ofisi.