Imefahamika kuwa, Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Cameroon Leandre Essomba Willy Onana ametua jijini Dar es salaam kwa siri kwa ajili ya kufanikisha dili la kujiunga na Simba SC.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 22 anatajwa kuwa mbini kujiunga na Wanamsimbazi akitokea Rayon Sports ya Rwanda, ambayo ameifungia mabao 16 msimu huu 2022/23.
Kiungo huyo ni kati ya wachezaji wanaotajwa katika usajili wa Simba SC kuelekea msimu ujao ambao utaanza kufanyika mara dirisha kubwa kufunguliwa hivi karibuni.
Mmoja wa mabosi wa Simba SC, amesema kiungo huyo ametua nchini na kuficha katika moja ya hoteli kubwa kwa ajili ya kufanya mazungumzo sambamba na kusaini mkataba.
Bosi huyo amesema mazungumzo hayo yapo katika hatua za mwisho kukamilika baada ya mchezaji mwenyewe kufikia muafaka mzuri wa kusaini mkataba wa miaka miwili.
Ameongeza kuwa, kiungo huyo amekubali kusaini mkataba huo wa miaka miwili baada ya ofa nzuri ambayo amewekewa mezani ili kukamilisha dili hilo.
“Muda wowote Onana atasaini Simba SC sambamba na kutambulishwa mara baada ya dili hilo kukamilika kwa asilimia kubwa huku mkataba wake ukiandaliwa kwa ajili ya kusaini.
“Huenda akawa mchezaji wa kwanza mpya kusajiliwa na Simba SC, na uzuri ni kwamba kocha mwenyewe anafahamu uwezo wa kiungo huyo ambaye amekuwa mfungaji bora wa ligi msimu huu.
“Onana yeye mwenyewe ameonesha nia kubwa ya kuichezea Simba SC ambayo anaamini itamtangaza kimataifa msimu ujao, wakati tukienda kucheza michuano ya kimataifa,” amesema bosi huyo.
Akizungumzia hilo la usajili, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema: “Wachezaji wengi wakubwa wanataka kuja kuichezea Simba, hiyo ni kutokana na ukubwa wa timu yetu.
“Ipo fedha ya kusajili mchezaji yeyote atakayehitajika na benchi la ufundi, yupo mwekezaji wetu Mo (Mohammed Dewji) ambaye ameweka pesa nyingi kwa ajili ya kufanya usajili.”