Mshambuliaji kutoka nchini Uruaguay Leandro Gastón Sirino Rodríguez, huenda akatimkia kwa mabingwa wa kihistoria barani Afrika Al Ahly, msimu ujao 2020/21.
Uwezekano wa mshambuliaji huyo wa klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kutimkia nchini Misri, umeibuliwa na wakala wake Joao Bittencourt, ambaye ameweka wazi kuwepo kwa ofa kutoka kwa miamba hiyo ya Misri.
Gastón mwenye umri wa miaka 29 amehusishwa na mipango ya kuwa mbioni kusajiliwa na mabingwa hao wa kihistoria Afrika, kufuatia kuwa kwenye kiwango bora tangu alipotua Mamelodi Sundowns akitokea FC Bolivar ya Bolivia Januari 2018.
Mshambuliaji huyo amecheza vyema kwenye Ligi ya Mabingwa barani Afrika na kuwa mchezaji aliye na nafasi kubwa wakati wa msimu wa 2019/20 kwa Masandawana, na Al Ahly tayari imetupa nyavu zake kumpeleka jijini Cairo kabla ya msimu ujao.
Imeripotiwa kuwa ofa ya kwanza ya Ahly ni Pesa na kumtoa Mshambuliaji wao wa Kimataifa wa Angola, Geraldo ambaye ameshindwa kufikia kiwango kilichotarajiwa na magwiji hao wa Cairo-Misri.
Tayari Geraldo ameshacheza michezo 10 bila kuhusika na goli lolote, na kama mambo yatakwenda kama yanavyotarajiwa atashuka bondeni (Afrika Kusini) ili kukamilisha uhamisho wa Gaston Sirino ambaye ameshaituikia Mamelodi Sundowns katika michezi 90 na kufungwa mabao 22 na kutoa pasi za mwisho 26.