Kiungo Leandro Trossard ana matumaini ya kucheza safu ya kiungo mshambuliaji lakini huenda Mikel Arteta asimpange nafasi hiyo anayoipenda msimu utakapoanza.
Arenal ipo bize kuhakikisha inampata Mohammed Kudus kutoka Ajax kwa Pauni 40 milioni anayecheza nafasi hiyo, hivyo itakuwa ngumu kwa Trossard.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji mara kwa mara alikuwa tishio akitokea benchi lakini Arteta alimpanga nafasi tofauti akiwa na uzi wa Arsenal.
Trossard anaweza kucheza winga zote mbili kama mshambuliaji, lakini nyota huyo hakuficha na kudai alijiunga na Arsenal akiwa na matumaini ya kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji.
Akizungumza kutokana na uamuzi wa Arteta wa kumchezesha nafasi tofauti alisema: “Ilinisaidia sana kwa sababu nimecheza nafasi tofauti. Nadhani wataangalia wapi nafiti zaidi. Nadhani Arteta anafahamu kwa sababu ni kocha mzuri.”
Lakini alipozungumza kuhusu nafasi yake halisi alisema: “Najisikia vizuri kucheza nafasi tofauti lakini kama wangeniambia kuchagua nafasi ningechagua kucheza nyuma ya mshambuliaji kwa sababu ndio napamudu zaidi. Lakini itategemea na mfumo wa timu.”
Kwa upande wa Martin Odegaard amekuwa na mchango mkubwa sana sehemu ya safu ya kiungo ya timu hiyo lakini Arteta akamwongeza kiungo mwingine Kai Havertz na watakuwa wakisiadiana.
Wakati huo huo Kudus anatolewa macho kwa hiyo kutakuwa na vita kubwa ya namba endapo Arsenal itafanikiwa kunasa saini yake.
Arsenal imepania kufanya makubwa kama msimu uliopita baada ya kushindwa kubeba ubingwa na kuipa mwanya Manchester City kunyakua kwa mara ya tatu mfululizo.