Lebanon imeanza leo maombolezo ya kitaifa ya siku tatu kufuatia mlipuko mkubwa ulioanzia katika bandari ya Beirut, Jumanne, Agosti 4, 2020 na kusababisha vifo vya watu 137, zaidi ya majeruhi 5,000 na watu 300,000 kupoteza makazi.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amewasili nchini humo leo akiwa ndiye kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kutembelea eneo lilokutwa na maafa.
Shirika la afya Duniani (WHO) limeahidi kutuma vifaa vya upasuaji kutoka Dubai, huku nchi mbalimbali zikiendelea kutuma msaada wa dharura. Moja kati ya nchi hizo ni Qatar ambayo imetuma hospitali za kuhamishwa, shuka za kufunikia majeruhi.
Algeria imetuma ndege nne na meli moja zikiwa na wahudumu wa afya na zimamoto wakati Ujerumani imetuma watalaamu wa shughuli za utafutaji na uokozi.
Chanzo cha mlipuko huo bado hakijabainika, inaaminika kuwa ulisababishwa na hifadhi ya tani 2,750 za kemikali ya ammonium nitrate ambayo imekuwa bandarini hapo kwa zaidi ya miaka mitano.