Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameweka wazi kile alichodai ni siri ya jinsi ambavyo Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete alivyomsaidia katika harakati za kurejea nchini kutoka Canada alikokimbilia.

Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara mjini Arusha, baada ya kupokelewa na umati wa wananchi akitokea nchini Canada, Lema alisema kuwa alimpigia simu Kikwete akimuomba amsaidie kumfikishia ujumbe Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kurejea nchini.

Lema ambaye alisimulia kuwa alitoroka nchini kupitia mpaka wa Namanga akielekea nchini Kenya na kisha kusafirishwa kama mkimbizi wa kisiasa Kwenda nchini Canada, anasema Rais huyo mstaafu alimuuliza “familia yako iko wapi,” akamjibu “niko nayo hapa na nimeweka ‘loud speaker’ wanakusikiliza.”

“Mheshimiwa Kikwete aliniuliza, ‘unataka kurudi lini’, nikamjibu nataka kurudi jana,” aliendelea kusimulia na kuongeza kuwa suala hilo aliliacha mikononi mwa Kikwete kwa muda huo na akamshukuru.

Aidha, mbunge huyo wa zamani alipongeza hatua za kidemokrasia zilizofikiwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan. Alitoa mfano akieleza kuwa baada ya kupata taarifa kwamba Rais ataingia Arusha kwa ajili ya mkutano maalum na mawaziri jana wakati naye anategemea kupokewa na wafuasi wa Chadema alipata wasiwasi, lakini mambo yalienda vizuri kwa ratiba zote.

“Mama, Mheshimiwa Rais naambiwa alipita pale akawapungia mkono wanachama wa Chadema ambao walikuwa wamekusanyika wakinisubiri. Hakuna aliyembeza, sanasana amejiongezea heshima zaidi… Rais anapita anawapungia mkono wanachama wa chama cha upinzani na mambo yanaendelea vizuri,” alisema Lema.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alimpa kazi Lema kukitangaza chama hicho katika Kanda ya Kaskazini kwa kishindo zaidi.

Rais Samia azitaka Wizara kujibu hoja
'Kigogo' ashtakiwa kwa mauaji, treni iliyoua 43 Ugiriki