Msimamizi Mkuu wa kituo cha treni cha Larissa nchini Ugiriki, ameshtakiwa kwa makosa ya kuua bila kukusudia baada ya ajali ya treni kusababisha vifo vya watu 43, wiki hii.

Umoja wa wafanyakazi wa Reli umeeleza kuwa unaamini mifumo ya usalama ya reli haikuwa inafanya kazi ipasavyo, na kwamba wamewahi kutoa tahadhari kwa miaka kadhaa.

Treni hiyo iliyokuwa imebeba watu 350, wengi wakiwa ni wanafunzi wenye umri wa kati ya miaka 20-29, waliokuwa wanasafiri kurejea masomoni mjini Thessaloniki baada ya kumaliza sikukuu ya kigiriki ya Orthodox Lent, iliharibika zaidi upande wa mbele.

Waziri Mkuu Kyriakos Mitsotakis amesema kuwa makosa ya kibinadamu ni sehemu ya sababu ya ajali hiyo, ingawa bado uchunguzi wa kina unaendelea. Serikali imetangaza siku tatu za maombolezo.

Mamia wameandamana nchini humo, wakikusanyika nje ya makao makuu ya kampuni inayowajibika na matengenezo ya reli za Ugiriki.

Wafanyakazi wa reli wamepanga kufanya mgomo leo, kwa kile wanachoeleza kuwa ni kulaani uzembe wa viongozi wa shirika la reli.

“Maumivu yamebadilika na kuwa hasira kwa ajili ya makumi ya watu waliofariki na kujeruhiwa ambao ni wafanyakazi wenzetu na wananchi wenzetu. Kitendo cha Serikali ya Ugiriki kutoheshimu miundombinu ya reli ndicho chanzo cha janga hili,” imeeleza taarifa ya umoja wa wafanyakazi wa reli.

Waziri wa Uchukuzi, Kostas Karamanlis amejiuzulu kufuatia ajali hiyo akieleza kuwa anawajibika kutokana na kushindwa kwa Mamlaka kurekebisha ipasavyo miundombinu ya reli.

Lema aanika siri, Kikwete alivyomsaidia kurejea nchini
Watoto wawili wajinyonga