Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema amesema anapanga kumtembelea aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya anayetumikia kifungo gerezani.
Mwanasiasa huyo aliyerejea nchini wiki hii akitokea Canada, amesema mpango wake ni kumjulia hali Sabaya ikiwezekana wikendi hii.
“Tena nimepanga kwenda kumtembelea Sabaya, inawezekana wikendi hii nitaenda,” alisema Lema kwenye mahojiano maalum na Millard Ayo.
Kiongozi huyo wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alitoa kauli hiyo alipokuwa anaeleza kuwa anaamini wapo viongozi wengi ambao walipaswa kufunguliwa mashtaka kama Sabaya lakini wako uraiani.
Alisema hatua ya kumshtaki Sabaya peke yake ni sawa na kuwa na wezi wawili wa TV, halafu mmoja pekee ndiye anayefunguliwa mashtaka na mwingine anaachiwa huru.
Alifafanua kuwa nia yake sio kutetea uhalifu, bali ni kutaka haki itendeke kwa kila aliyeshiriki kufanya vitendo viovu kwa kutumia madaraka aliyopewa.
Lema ameeleza kuwa anaamini wapo viongozi wengine ambao watafunguliwa mashtaka kwa makosa waliyoyafanya walipokuwa na dhamana za uongozi.