Mtoto wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ametakiwa kujibu shtaka analotuhumiwa la kutangaza nia yake ya kuwania urais nchini humo akiwa bado anahudumu katika jeshi la nchi hiyo.
Katika kesi iliyowasilishwa kwa Mahakama ya kikatiba ya Uganda na Wakili wa haki za binadamu Gawaya Tegulle, aliiomba mahakama hiyo iliyoko mjini mkuu, Kampala, kumzuia Jenerali Kainerugaba kufanya shughuli za kisiasa akiwa bado anatumikia jeshi.
Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Monitor, Gawaya pia anataka jenerali huyo ashtakiwe kwa uhaini kufuatia madai dhidi yake kupanga njama ya kumrithi baba yake akitumia mbinu “haramu”.
Mahakama imempa Jenerali Kainerugaba ambaye ni kamanda wa jeshi la nchi kavu la Uganda, muda wa siku 10 kuwasilisha majibu yake.
Inakumbukwa kwamba mnamo tarehe 2 Mei, Kainerugaba alitangaza kuzindua mipango yake kisiasa huku akichochea uvumi kwamba alinuia kumrithi baba yake ambaye ni rais wa muda mrefu nchini Uganda.
Kainerugaba vile vile alitangaza mnamo Machi 8, 2022, kustaafu kwake kutoka jeshi lakini Rais Museveni alikataa.
Kainerugaba ni miongoni mwa wanajeshi wa Uganda waliopanda vyeo haraka na kupandishwa huko kuliibua fununu kwamba anaandaliwa kuwa mrithi wa Museveni ambaye ametawala Uganda kwa zaidi ya miaka 30.
Hata hivyo, Rais Museveni mwaka wa 2013 alijitokeza kukanusha madai hayo akisema: “Uganda sio nchi ya kifalme ambao uongozi unarithishwa kutoka kwa baba kwenda kwa mtoto. Hili linalosemwa ni [Muhoozi] ni mradi ni maneno tu yakutungwa na watu.”
Lakini tetesi hizo ziliendelea kuenea zaidi mwaka wa 2017, Muhoozi alipoteuliwa kuwa mshauri wa rais wa shughuli maalumu. Cheo hicho ambacho kilimsongeza Ikulu, kilichochea fununu kwamba Kainerugaba ananolewa kuwa rais mtarajiwa wa Uganda.
Kando na vyeo vyake, kijana huyo wa Museveni amekuwa akishutumiwa na wadogo zake kwa vitendo vingi vya unyanyasaji na utesaji wa watu hususana wanaokosoa na kupinga utawala wa baba yake.