Mashambuliaji kutoka nchini Burundi na klabu ya DTB, Amissi Tambwe amekiri akuwa katika wakati mgumu, katika harakati za kuapmabania kuipandisha daraja klabu hiyo, ambayo imedhamiria kucheza Ligi Kuu msimu ujao 2022/23.
Klabu ya DTB imekua na muonekano mzuri wa kiushindani kufuatia usajili mkubwa walioufanya mwanzoni mwa msimu huu, na tayari imeanza vyema Mshike Mshike wa Ligi Daraja la Kwanza.
Tambwe ambaye aliwahi kuzitumikia klabu nguli za Tanzania (Simba SC na Young Africans) amesema anakutana na mazingira magumu katika michezo ya Ligi Daraja la Kwanza aliyocheza mpaka sasa, na amejiridhisha ligi hiyo ina changamoto kubwa ya ushindani na mbinu chafu.
Amesema kuwa changamoto kubwa ambayo anakumbana nayo katika Ligi Daraja la Kwanza ni kuchezewa mpira wa kihuni kutokana na ligi hiyo kutoonyeshwa kwenye televisheni.
Tambwe mpaka sasa amefanikiwa kuifungia DTB mabao sita katika michezo minne aliyocheza katika Ligi Daraja la Kwanza.
Tambwe amesema kuwa kwenye Ligi Daraja la Kwanza mabeki wa ligi hiyo wamekuwa wakicheza mpira wa kihuni kwa kuwa wanafahamu kuwa hawaonekani popote tofauti na ligi kuu jambo ambalo linawaumiza sana washambuliaji wa ligi hiyo.
“Ligi daraja la kwanza kuna uhuni sana unafanyika haswa kwa mabeki wengi hucheza soka la ajabu huku wakiamini kuwa hawaonekeni sehemu yeyote kwa kuwa ligi hiyo haionyeshwi kwenye televisheni.
“Kwenye ligi kuu ni ngumu mabeki wengi kucheza mpira wa kihuni kwa kuwa wanafahamu kuwa wanaonekana na ligi inaonyeshwa kwenye televisheni tofauti na ligi daraja la kwanza, kwa kweli washambuliaji tunaumizwa sana,” amesema Tambwe.
Klabu ya DTB inaongoza msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza kwa kufikisha alama 8, baada ya kushinda michezo miwili na kutoka sare michezo miwili.