Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara (VPL), itaendelea tena mwishoni mwa juma hili, huku mchezo mmoja ukitarajiwa kuchezwa kesho Ijumaa Novemba 3, 2017 kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea ambapo wenyeji Majimaji FC watacheza na Stand United ya Shinyanga.
Mchezo huo utakaopigwa kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma umepangwa kuanza saa 10.00 jioni (1600h).
Jumamosi kutakuwa na michezo mitano ambapo minne itaanza saa 10.00 jioni (1600h) wakati mwingine utakuwa saa 1.00 usiku (1900h).
Michezo hiyo ya Jumamosi itakuwa ni kati ya Singida United itakayocheza na Young Africans kwenye Uwanja wa Namfua mkoani Singida wakati Tanzania Prisons itakuwa wageni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera.
Njombe Mji kwa upande wao watakuwa wenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe huku Mtibwa Sugar wakisafiri kutoka Morogoro kwenda Mtwara kucheza na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona. Hiyo ni michezo itakazochezwa saa 10.00 jioni.
Mchezo pekee utakaofanyika saa 1.00 usiku utakuwa kati ya Azam FC na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Azam.
Jumapili kutakuwa na michezo miwili ya Ligi Kuu ambapo Lipuli ya Iringa itakuwa mwenyeji wa Mwadui FC ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Samora wakati Simba watakuwa mgeni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Mechi hizo zitaanza saa 10.00 jioni.