Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea leo Ijumaa (Desemba 18) kwa michezo mitatu kuchezwa kwenye viwanja tofauti, huku Azam FC wakitarajia kukutana uso kwa macho na maafande wa Ruvu Shooting kutoka Mlandizi mkoani Pwani.
Mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi, utakua wa pili kwa kocha George Lwandamina tangu alipoanza kukaa kwenye benchi mwanzoni mwa juma hili walipokutana na Namungo FC, huku matokeo yakiwa mabao mawili kwa mawili.
Mchezo mwingine wa Ligi Kuu utakaochezwa leo Ijumaa utashuhudia Mwadui FC wakicheza nyubani Mwadui Complex dhidi ya Maafande wa Jeshi la Polisi (Polisi Tanzania) kutoka mkoani Kilimanjaro, huku Biashara United Mara wakiwakaribisha nyumbani mjini Musoma Mbeya City FC kwenye uwanja wa Karume.
Mkoani Kagera katika mji wa Bukoba, wakata miwa kutoka Wilaya ya Isenyi Kagera Sugar, watakua na shughuli pevu kwenye uwanja wa Kaitaba, pale watakapo papatuana na Coastal Union kutoka jijini Tanga.
Ligi Kuu Itaendelea tena kesho Jumamosi (Desemba 19) kwa michezo mingine minne, ambapo Gwambina FC watakua nyumbani Gwambina Complex wilayani Misungwi mkoani Mwanza wakicheza dhidi ya Maafande wa Jeshi la Magereza (Tanzania Prisons), huku Ihefu FC watawasubiri KMC FC kutoka Dar es salaam kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mtibwa Sugar wataendelea kuwa nyumbani mkoani Morogoro kwenye uwanja wa Jamhuri wakicheza dhidi ya JKT Tanzania kutoka mkoani Dodoma, na vinara wa msimamo wa ligi hiyo Young Africans kwa mara ya kwanza watacheza jijini Arusha kwenye uwanja wa Sheikh Amri Kaluta Abeid dhidi ya Dodoma Jiji FC.