Mshambuliaji na nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi, ameomba aachwe katika kikosi cha timu ya taifa hilo, ambacho kitatajwa wakati wowote juma lijalo, kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Colombia, utakaochezwa mapema mwezi ujao.
Messi amewasisha ombi hilo kwa viongozi chama cha soka nchini Argentina (AFA), kwa kuhitaji muda wa kupumzisha akili yake kwa kipindi chote cha mwaka 2018 kilichosalia.
Maamuzi ya mshambuliaji huyo yanakuja, kufuatia kikosi cha Argentina kushindwa kufikia malengo yake, wakati wa fainali za kombe la dunia 2018 zilizofanyika nchini urusi, huku Messi akiwa miongoni mwa wachezaji walioitwa kikosini.
Argentina ilitolewa kwenye michuano hiyo na mabingwa Ufaransa kwa kufungwa mabao manne kwa matatu, katika hatua ya 16 bora, huku ikionyesha udhaifu mkubwa kwenye hatua ya makundi kwa kulazimishwa sare na Iceland kabla haijafungwa na Croatia, na baadae kushinda dhidi ya Nigeria.
Kocha wa muda wa timu ya taifa ya Argentina Lionel Scaloni amethibitisha kupata ombi la Messi, alipozungumza na kituo cha televisheni cha TNT Sports, na ameliafiki.
Hata hivyo haijafahamika kama Lionel Messi atakua tayari kurejea katika kikosi cha Argentina mwanzoni mwa mwaka ujao, hali ambayo inaendelea kuzua hofu miongoni mwa mashabiki wa soka nchini humo.
Baada ya fainali za kombe la dunia 2018, tetesi za kustaafu soka la kimataifa kwa mshambuliaji huyo wa FC Barcelona ziliibuliwa na vyombo mbali mbali vya habari, jambo ambalo Messi hakuwahi kulithibitisha.