Nahodha na mshambuliaji wa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona Lionel Messi, ameanza kufanya mazoezi na wachezaji wenzake, baada ya kuwa nje kwa majuma kadhaa yaliopita.
Messi amerejea mazoezini huku FC Barcelona wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao matano kwa mawili dhidi ya Valencia, uliopatikana usiku wa jumamosi kwenye uwanja wa Camp Nou.
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Argentina, alikua akisumbuliwa na majeraha ya kiazi/kigimbi cha mguu, na tangu msimu wa 2019/20 ulipoanza alikua akiwashuhudia wenzake akiwa jukwaani.
Leo jumatatu, Messi anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachosafari hadi mjini Dortmund huko Ujerumani, kwa ajili ya mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, utakaochezwa kesho jumanne.
Hata hivyo meneja wa FC Barcelona Ernesto Valverde, hajathibitisha kama ataweza kumtumia mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 32, katika mchezo dhidi ya Dortmund.
“Bado ninaendelea kumfuatilia kwa ukaribu, kama atakua katika kiwango cha kuridhisha mazoezini huenda nikamtumia katika mchezo wetu ujao, lakini kwa sasa ninaona ni vyema tukampa muda, hadi siku ya mchezo,” alisema Valverde.
“Nanatambua kila shabiki wa FC Barcelona angetaka kumuona tena Messi akirudi uwanjani na kuisaidia timu, halikadhali hata mimi kama meneja ninataka iwe hivyo, lakini jambo kubwa tunapaswa kusubiri, kama atatudhihirishia yupo tayari, tutamtumia.” Aliongeza kocha huyo kutoka Hispania.