Nahodha na Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Argentina Lionel Messi amethibitisha kuwa “hafikirii” kama atacheza Fainali za Kombe baada ya kuliongoza taifa lake kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mwaka jana nchini Qatar.
Messi ambaye ana umri wa miaka 35 amesema hayo katika mahojiano na vyombo vya habari vya China kuhusu mustakabali wake kwenye michuano hiyo mikubwa ambayo inayofuata itafanyika mwaka 2026 kwa ushirikiano wa nchi tatu, Marekani, Canada na Mexico.
“Nimesema mara kadhaa hapo awali kwamba sifikirii hivyo, kwamba hiyo (2022) lilikuwa Kombe langu la mwisho la Dunia,” amesema alipoulizwa na Titan Sports ya China kwenye mahojiano.
“Nitaona jinsi mambo yanavyokwenda, lakini kwa nadharia sidhani kama nitakuwepo kwa Kombe lijalo la Dunia,” ameongeza.
Mshindi huyo mara saba wa tuzo ya Ballon d’Or kwa sasa yuko jijini Beijing nchini China ambako Argentina itacheza mechi ya kirafiki na Australia leo Alhamisi.
Argentina itacheza mechi hiyo ya kirafiki kwenye Uwanja wa Workers unaochukua watu 68,000 mjini Beijing. Messi atatimiza miaka 39 wakati wa mashindano yajayo.
Messi juma lililopita alitangaza kujiunga na klabu ya Inter Miami inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani, MSL, baada ya mkataba wake wa miaka miwili na Paris Saint-Germain kukamilika.
Mechi hiyo ni marudio ya mchezo wa hatua ya 16 bora kati ya timu hizo kwenye Kombe la Dunia mjini Doha, ambapo Argentina ilishinda 2-1.
Huku mashabiki wa China wakitamani kumuona nyota huyo wa zamani wa Barcelona akicheza, tiketi zimeuzwa mapema na haraka licha ya kuuzwa kwa bei ya juu hadi Yuan 4,800 (Dola 671) sawa na Sh. 1,600,335.