Gwiji wa ukufunzi wa soka nchini Italia Marcello Lippi, ametangaza kuachana na kazi hiyo aliyoitumikia kwa miaka 38, (akianza mwaka 1982) akiwa na kikosi cha vijana cha klabu ya Sampdoria.
Lippi aliyeiwezesha Italia kutwaa ubingwa wa dunia mwaka 2006, ametangaza maamuzi hayo baada ya kukaa kwa muda mrefu bila ya kuwa na kibarua cha ukufunzi.
Mwaka 2019 ilikua mara ya mwisho kwa kocha huyo kufanya kazi za ukufunzi akiwa na timu ya taifa ya China, ambayo alishindwa kuiwezesha kuendelea na kampeni za kusaka tiketi ya kushiriki fainali z kombe la dunia 2022, kwa kufungwa na Syria.
Lippi mwenye umri wa miaka 72, pia amewahi kuvinoa vikozi vya klabu kadhaa vya nchini kwao Italia kabla ya kutimkia China kukinoa kikosi cha klabu ya Guanzhou Evergrande.
“Nimemaliza kazi ya kufundisha soka, sasa inatosha.” Lippi aliambia Radio Sportiva.
“Labda naweza kutumika katika majukumu mengine acha tuone.
Klabu alizozifundisha tangu mwaka 1982 ni Sampdoria (Timu ya vijana) 1982–1985, Pontedera 1985–1986, Siena 1986–1987, Pistoiese 1987–1988 , Carrarese 1988–1989, Cesena 1989–1991, Lucchese 1991–1992, Atalanta 1992–1993, SSC Napoli 1993–1994, Juventus 1994–1999, Inter Milan 1999–2000 na Juventus 2001–2004 na Guangzhou Evergrande 2012–2014.
Upande wa timu za taifa alianza mwaka 2004 akiwa na timu ya taifa ya Italia mwaka 2006, na kazi hiyo alidumu nayo hadi mwaka 2010, na kisha akakinoa kikosi cha China kuanzia mwaka 2016 hadi 2019.
Mafanikio aliyoyapata:
Lippi alichukua nafasi ya kuifundisha timu ya Juventus mwaka 1994 na kuiongoza The Bianconeri kushinda mataji matatu ya Serie A na taji la ligi ya mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) msimu wa 1995-1996.
Lippi akiwa nchini Italia alifanikiwa kupata mafaniko kama kushinda taji la Serie A mara tano, Italiana Supercoppa nne, Champions League UEFA Super Cup, Intercontinental Cup na Coppa Italiana.
Baada ya kuondoka Juventus mwaka 2004 Lippi aliisadia Italia kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2006 pia alichaguliwa tena na Azzurri baada ya kukaa miaka miwili bila kuifundisha timu ya taifa.
Akiwa China, Lippi alijiunga na Guanzhou Evergrande mwaka 2012 na kushinda mataji matatu ya Chine Super League na AFC Champions League sambamba na mafanikio ya FA Cup na Chinese FA Super Cup.